TAMKO RASMI
(English)

Tarehe: 29 Aprili 2010
close window


TAMKO LA DODOMA
(Download)

1.     UTANGULIZI 

1.1      Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), linamshukuru Mungu kwamba katika hekima yake isiyopimika, na kwa njia ya Mwana wake Yesu Kristo, ametuunganisha waumini wake wote ulimwenguni kuwa mwili mmoja na hivyo kutufanya tuhusiane. Kwa njia hiyo, tunaweza kutembea pamoja na kufanikishwa katika mambo mengi. 

1.2      Katika uhusiano wetu kama mwili mmoja, tumeshirikiana kwa njia mbalimbali katika mambo magumu na mepesi. Kilichotuwezesha kudumu pamoja hadi sasa, kwa msaada wa Mungu, ni kutambua na kukumbuka kwamba kila siku ya ibada, katika maisha ya Kanisa, tunakiri kuwa Kanisa la Mungu ni moja, takatifu, la ulimwenguni pote na la Kimitume. Hivyo, tukio lolote katika kanisa mojawapo, lisilo la kawaida katika misimamo na mafundisho yaliyozoeleka kwa karne nyingi katika Kanisa zima la Mungu, ni lazima litaamsha mshtuko na itikio la aina moja au nyingine kutoka makanisa mengine duniani pote. 

1.3      Kwa wakati uliopo, mojawapo ya matukio yasiyo ya kawaida, kwa mtazamo na uelewa wa KKKT, ni hilo la baadhi ya makanisa -- hasa kule Ulaya na Marekani -- kuamua kuhalalisha ndoa za watu wa jinsia moja. Katika kufanya hivyo, sababu mbalimbali zinatolewa na makanisa husika kutetea uamuzi wao huo. Hapa tutaje tu, kwa muhtasari, baadhi ya sababu zinazotolewa na makanisa hayo.

1.3.1    Kwamba eti mafundisho ya Kanisa kuwa ndoa, kulingana na  Maandiko Matakatifu, ni kati ya mwanaume na mwanamke si kama inavyofafanuliwa.  Kwa msingi wa hoja kama hii, hao wanaotetea ndoa za watu wa jinsia moja wameanza kufanya kila wanaloweza kubomoa kifungu kimoja baada ya kingine kinachoonyesha kwamba ndoa halali, kibiblia, ni kati ya mwanaume na mwanamke. Wanafanya hivyo kwa kuleta tafsiri zao "mpya na yamkini potofu" - tofauti na msimamo na uelewa wa Kanisa uliodumu miaka mingi kuhusu maana ya ndoa kulingana na mafundisho ya Neno la Mungu. Baadhi ya vifungu vya Biblia vinavyopigwa vita na kupewa tafsiri nyingine na wapenda ndoa za watu wa jinsia moja ni hivi vifuatavyo: Mwanzo 1:27-28; 2:24; Mt. 19: 5-6a; Rum. 1:26-27a na Gal. 3:28.

1.3.2       Kwamba eti kilicho muhimu, kwa habari ya mahusiano kati ya wawili wahusika katika mahusiano ya kindoa au namna nyingine za mahusiano ya kimapenzi ni upendo.  Mradi watu wanapendana, mahusiano kama hayo ni sahihi na halali --ndivyo wanavyodai watetezi wa ndoa kati ya watu wa jinsia moja.

1.3.3       Kwamba eti   mazingira na tamaduni zao za wakati huu ni tofauti na za wakati uliopita kuhusu maana na mtazamo juu ya nini halali na nini si halali kwa mahusiano ya kindoa na kimapenzi. Wanaongeza kudai kuwa suala la maadili kuhusu nini ni dhambi na nini si dhambi, hubadilika kulingana na wakati na mazingira ya mahali mtu alipo. Kwa macho yao, mtazamo wa jamii juu ya maadili, hasa kuhusiana na suala la mahusiano kindoa au kimapenzi kati ya watu wa jinsia moja au jinsia tofauti, umebadilika, na wanalitaka Kanisa nalo liende na wakati katika mtazamo ama msimamo wake kuhusu mambo haya. Kadhalika wateteaji wa mambo haya wanadai kwamba, "Tabia za kukemea na kukunjia uso mambo ya  ndoa za watu wa jinsia moja zimepitwa na wakati,"  Hivyo, wanatutaka sisi wengine  wote katika Kanisa la Mungu na jamii ya ulimwengu kwa ujumla tukubali kubadilika na kwenda na wakati, kama wao,  katika  mazingira haya mapya! 

1.3.4       Kwamba eti kwa kuwa sheria za nchi hizo yaliko makanisa yanayotetea na kuhalalisha ndoa za watu wa jinsia moja zimebadilika na kuwa upande wa ndoa za aina hiyo, makanisa katika nchi hizo yangejikuta mahali pagumu sana katika kazi na maisha yao kama yangeng'ang'ania msimamo wao wa miaka yote iliyopita kuhusu ndoa kati ya watu wa jinsia moja, na masuala mengine ya mahusiano kati ya watu wa jinsia hiyo moja. Maana yake, kwa tafsiri yetu, makanisa hayo yameamua kukubaliana na hatua zilizochukuliwa na mamlaka za nchi zao kama njia ya maridhiano ili hayo makanisa yasije yakapoteza maslahi yao fulani katika suala zima la ndoa endapo yangeendelea kushikilia msimamo wao wa miaka yote iliyopita -- yaani, kupinga na kukataa uhalali wa ndoa za watu wa jinsia moja. 

1.3.5       Kwamba eti suala la mahusiano --kindoa au kujamiiana ki-namna nyingine - kati ya watu wa jinsia moja, ni uamuzi kati ya watu wawili wanaohusika; wana uhuru kuamua kufanya wapendavyo katika hili. Kwa hiyo dai la msingi ni kwamba siyo sawa kwa yeyote kuwaingilia katika mambo yao hayo, bali kuwaacha huru wafanye kama wapendavyo.  Kuna sababu nyingine nyingi kama zilizotajwa hapo juu, zinazotolewa ama kwa maelezo ya mdomo na kalamu au kwa vitendo, na makanisa yaliyohalalisha ndoa za watu wa jinsia moja.

 

2.        HOJA MBADALA  

2.1   Kuhusu hoja zitolewazo na watetezi wa ndoa za watu wa jinsia moja, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania lina mtazamo na msimamo tofauti. Halikubaliani na sababu zozote zinazotolewa na watetezi wa ndoa za aina hiyo na uhalalishwaji wake.

2.2 Kanisa hili, (KKKT), linasimama juu ya msingi wa Neno la Mungu kwamba maana ya ndoa ni kama inavyofundishwa katika vifungu vya Biblia vilivyotajwa sehemu ya 1.3.1 hapo juu.  Vifungu ambavyo vimeanza kupewa maana na tafsiri tusiyoweza kuikubali. Sisi na wengine wote duniani pote walio na msimamo kama wetu katika suala hili la kupinga ndoa za watu wa jinsia moja, tunaamini kuwa Biblia haitafsiriwi kama wapendavyo watu fulani au mamlaka fulani ama utamaduni fulani bali hujitafsiri yenyewe kwa lugha mbalimbali kwa usahihi wake usiobadilika.

2.3 Kanisa hili linaamini kwamba upendo ni kiini cha mapenzi na uhusiano wa kweli kati ya watu wawili wanaoishi, au wanaotaka kuishi pamoja, katika ndoa. Lakini, kwa habari ya kuoa na kuoana , upendo huu ni kati ya watu wawili wa jinsia tofauti. Aidha, KKKT inaelewa kuwa somo juu ya upendo ni pana sana, na kwamba kuna maadili maalumu kuhusu matumizi sahihi ya karama hii ya upendo au kupendanaKanuni za maadili kuhusu maana sahihi ya upendo na matumizi yake zinapokiukwa au kuanza kupindishwapindishwa kwa sababu yoyote ile, basi upo uwezekano mkubwa wa binadamu kujikuta katika hali ambapo neno upendolinatumiwa kumaanisha na kuhalalisha kila aina ya uhusiano hata kama haukubaliki kibiblia na kijamii.  Hali kama hiyo ikiruhusiwa, ya kudai eti mradi upendoupo kati ya watu wawili wahusika, basi ndoa ya aina yoyote inakubalika. Hoja hii ikikubalika Kanisa na jamii kwa ujumla tunaweza kujikuta mahali ambapo tunaanza kuridhia na kutetea  ndoa hata kati ya wana ndugu, wazazi na watoto na pengine hata kati ya binadamu na wanyama -- si mradi kinachowaunganisha  hao viumbe wawili ni kitu kinachoitwa upendo! Haidhuru ni tafsiri gani inatolewa? Tunachotaka kusisitiza hapa ni kwamba, tuwe waangalifu sana tunapozungumzia neno upendo hata kudiriki kufanya kuwa kigezo muhimu na pekee kuliko vyote katika suala la ndoa.

2.4  Jibu lililotangualia, hapo juu, linahusu pia uhalalishwaji na ushabikiaji wa ndoa za watu wa jinsia moja kwa hoja kwamba katika tamaduni na jamii za watu wa nchi zile ambako ndoa za watu wa jinsia moja zimehalalishwa, pamekuwapo mabadiliko makubwa katika fikra za watu. Watu hawaoni tena kwamba ni vibaya wala kutokuwa halali kwa watu wa jinsia moja kuoana. Utamaduni wao wa sasa una mwelekeo unaounga mkono ndoa za jinsi hiyo. Mtazamo wa kimaadili wa sasa ni tofauti na wa wakati uliopita. KKKT inakubali kuwa ni kweli misimamo fulani ya kimaadili inaweza kubadilika kulingana na watu wako wapi na ni wakati gani. Lakini waumini wa KKKT wanajua na kuamini kuwa kuna mambo yasiyobadilika, kama vile pua kutobadilika kuwa mdomo au masikio kuwa macho.

2.5  Ni kweli kuwa maadili yaliyoangaliwa na jamii kwa mwelekeo hasi miaka iliyopita, sasa yanaangaliwa kwa mwelekeo wa chanya au kuridhia. Ni dhahiri kuwa wakati wa sasa ni tofauti, na jamii imebadilika katika mwelekeo na mtazamo wake katika mambo mengi. Lakini ni kweli, vilevile, kwamba maadili na msimamo wa Kanisa na wa jamii kwa ujumla, haviwezi kuwa na misingi ya kimaadili inayoyumbayumba wakati wote. Ni lazima Kanisa na jamii viwe na kanuni za kimaadili zinazoweza kuhimili mabadiliko ya kijamii, kisayansi, kisiasa, kiuchumi, nk. Kanisa hili linaamini kuwa, kwa msingi wa mafundisho ya Neno la Mungu, yako maadili yasiyopaswa kubadilishwa na kupindishwa pindishwa na misukumo ya mabadiliko ya wakati, hali na mahali. Mojawapo katika hayo, yahusu suala la ndoa na maana yake. Aidha kukubali ndoa za watu wa jinsia moja ni kuhujumu msingi wa agizo la Mungu kuhusu uumbaji unaoendelea.

2.6 Aidha, mabadiliko ya kimaadili katika jamii moja, mahali fulani, tuseme Ulaya na Marekani, yasichukuliwe kama ndio mwongozo kwa mabadiliko mahali pengine pote ulimwenguni. Wala mabadiliko yao ya  kitamaduni, kijamii, nk, katika nchi za Ulaya na Marekani yasilazimishwe juu ya watu wa nchi nyingine au makanisa katika nchi hizo. Kwa sababu hao watu wa sehemu nyingine, nje ya Ulaya na Marekani, pia wana misingi yao ya kijamii inayolinda maadili yao. Sisikama Watanzania/Waafrika, tuna maadili yetu yaliyojengwa juu ya misingi ya tamaduni zetu bayana ambazo zinatambua mahusiano, ki-ndoa, kati ya watu wa jinsia tofauti tu. Kwa hiyo, kama watu wengine watasema kwamba wanahalalisha ndoa za watu wa jinsia moja kwa kuwa mazingira mapya ya mahali na wakati walipo yanaruhusu hayo, basi ieleweke kuwa mazingira ya wakati na tamaduni zetu hayaruhusu mambo hayo.

2.7 Hoja ya kwamba ndoa au mahusiano kati ya watu wa jinsia moja ni jambo la watu wawili, ni hoja ya upande mmoja. Kwetu sisi waumini wa KKKT kwa upande wa pili tunabainisha kuwa hilo siyo tukio kati ya watu wawili tu bali inaeleweka daima kuwa wao ni sehemu ya familia na jamii pana zaidi. Hao wawili hawawezi kuruhusiwa kujifanyia mambo hata yasiyokubalika na jamii, kwa kinga ya: "Tuache peke yetu, msituingilie katika mambo yetu; haya ni mambo yetu wenyewe, na ni uamuzi wetu wenyewe kufanya tulivyoamua kufanya," nk. Hapana! Katika Kanisa na jamii kwa ujumla, kwa kadiri tunavyohusika katika mazingira na utamaduni wetu, kuna mambo ambayo binadamu yeyote, haidhuru yuko wapi, sharti atambue kuwa yeye si peke yake na wala hapaswi kuishi kwa nafsi yake tu katika mambo yote na wakati wote. Ndivyo ilivyo katika suala hili la ndoa za watu wa jinsia moja.

 

3.      HITIMISHO  

3.1 Kwa hiyo basi, kwa msingi wa ufahamu wa Kanisa moja, na kwa kuona ulazima wa kuongoza Kanisa kichungaji, kwa kufuata ufahamu wa Neno la Mungu na maungamo yake.  Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania linapenda kuonyesha bayana msimamo wake wa sauti ya kinabii, kuhusiana na suala la ndoa za watu wa jinsia moja, kwamba ni msongo mwitu na mwiba mkali katika mwili wa Bwana Yesu Kristo (1 Kor. 12: 12-27) unaosababisha jeraha lenye maumivu makali kwa wana KKKT na wengine wengi wa mahali pengine ulimwenguni pote wenye msimamo kama wetu katika suala hili, katika ngazi mbalimbali za uhusiano na mfumo wa uongozi.

3.2  Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania linaona kuwa maamuzi yoyote ya upande mmoja yasiyoendana na uelewa na mtazamo wa pamoja katika suala la ndoa kati ya watu wa jinsia moja yanadhoofisha umoja wa Kanisa lote kama mwili wa Kristo.

3.3  Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania bado linakataa utumiaji usio sahihi na tafsiri potofu za Maandiko Matakatifu ili kuhalalisha ndoa za watu wa jinsia moja.

3.4 Tunaamini kwamba hakuna sehemu yoyote ya Kanisa la Mungu inayoweza kufaulu kutatua mambo yake yote peke yake, bila nguvu ya pamoja ya mwili mzima wa Kristo. Kama isemwavyo: Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu. Jambo hili la maamuzi kuhusu kuhalalishwa kwa ndoa za watu wa jinsia moja, limeonyesha dhahiri kwamba nguvu ya umoja wetu imedhoofishwa.

3.5 Bila shaka haitoshi wala haisaidii tukiishia katika kulaumiana na kuhukumiana kutokana na tofauti zetu juu ya suala hili. Busara na hekima ya Roho Mtakatifu, itusukume kuzama katika maombi, toba, kuendelea kushauriana, kuonyana na kusaidiana katika roho ya upendo wenye misingi ya Neno la Mungu (Kol. 3:5-17).

3.6 Tunapenda kuwatia moyo na kuwaunga mkono kwa dhati wale wote, katika makanisa yote ulimwenguni -- wawe wengi au wachache -- wanaopinga, uamuzi wa kuhalalisha ndoa za watu wa jinsia moja. Tunatoa wito kuwa, sisi sote kwa pamoja tuendelee kuwa chumvi na nuru katika uhusiano wetu, tukielekeza nguvu zetu katika kudumisha umoja na ushirikiano kati yetu. Umoja utatuwezesha kutoruhusu tena hali itakayoleta majeraha zaidi kwenye mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

3.7 Tunaona kwamba hizi ni nyakati za uovu unaotafuta kulididimiza Kanisa la Mungu. Kwa hiyo tunatoa wito kwa waumini wote wa KKKT na makanisa mengine yenye msimamo kama wetu kuomba kwa dhati na kutunza ushuhuda wa mtu binafsi na wa Kanisa zima la Mungu.

3.8 Tunatoa tahadhari kwa kila muumini wa KKKT kuwa makini sana katika kupambanua na kuyakataa mafundisho mageni ambayo yanaweza kuwapotosha kwa urahisi waumini katika ulimwengu huu wa utandawazi.

3.9 Katika hali halisi ya ushirikiano kati yetu na makanisa mengine ya Ulaya na Marekani, na mahali pengine, msimamo wa Kanisa hili umewekwa bayana katika majibu kwa hojaji iliyoandaliwa na Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani (FMKD) kuhusu ubadilishanaji wa watumishi. Kwa kuwa lengo la hojaji hiyo na maamuzi yatakayofanywa hatimaye na FMKD kutokana na majibu yaliyotolewa na makanisa mengine wanachama yanatuhusu sisi pia;

3.9.1    Sisi KKKT kama wanachama tunasema kwamba Kanisa letu halitakuwa tayari kuingia katika mabadilishano ya watu yanayojumuisha wale walio katika ndoa za jinsia moja au wale wanaoshabikia ndoa za jinsi hiyo na uhalalishwaji wake.  Kwa maneno ya wazi zaidi, maana yake ni kwamba walio katika ndoa za jinsia moja, na wanaoshabikia ndoa za jinsi hiyo na uhalalishwaji wake, hawakaribishwi kufanya kazi katika KKKT. KKKT haitakuwa tayari kubadilisha msimamo wake kuhusu suala hili hata kwa ushawishi na au shinikizo la nguvu ya fedha.

3.9.2    Hata katika ushirikiano wake na wengine kwa njia ya vyombo vya ushirikianao kama LWF, WCC, LMC na/au mashirka mengineyo (ya kidini na yasiyo ya kidini) n.k., KKKT haitaunga mkono mbinu zozote za kujaribu kuwapigia debe na kuwapenyeza katika mashirika hayo watu walio katika ndoa za jinsia moja au washabiki wa ndoa za watu wa jinsia moja, na aina zote za vitendo vya kishoga.

3.10   KKKT haiwezi kuwalazimisha watu wa Ulaya au Marekani, waone na kufanya kama sisi katika suala hili la ndoa za watu wa jinsia moja; lakini inaweza kuwaeleza msimamo wake kinaganaga kuhusu suala lenyewe.  Inaamini kuwa upande mwingine pia utajali na kuheshimu msimamo wake kamaunavyoelezwa katika tamko hili. Aidha, KKKT inategemea kuwa marafiki zake, popote pale walipo, ambao, lakini, inatofautiana nao sana sasa katika suala hili la ndoa za watu wa jinsia moja, hawatajaribu- na ingeomba wasijaribu- kwa namna yoyote ile, wakati wowote ule, mahali popote pale, kuujaribu msimamo wake dhidi ya ndoa za watu wa jinsia moja, ikiwa ni pamoja na vitendo vya namna zote za kishoga.  

 

Limewekwa saini na:

Maaskofu wa KKKT

1.       Askofu Dk. Alex Gehaz Malasusa, KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani na
          Mkuu, KKKT

2.       Askofu Andrew Gulle, KKKT Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria

3.       Askofu Thomas Laiser, KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati

4.       Askofu Michael Adam, KKKT Dayosisi Mkoani Mara

5.       Askofu Festo Ngowo, KKKT Dayosisi ya Dodoma

6.       Askofu Dk. Owdenburg M. Mdegella, KKKT Dayosisi ya Iringa

7.       Askofu Dk. Benson K. Bagonza, KKKT Dayosisi ya Karagwe

8.       Askofu Dk. Martin Shao, KKKT Dayosisi  ya Kaskazini

9.       Askofu Elisa Buberwa, KKKT Dayosisi ya Kaskazini Magharibi

10.    Askofu Dk. Stephen I. Munga, KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki

11.    Askofu Eliuphoo Sima, KKKT Dayosisi ya Kati

12.    Askofu Dk. Israel-Peter Mwakyolile, KKKT Dayosisi ya Konde

13.    Askofu Cleopa A. Lukilo, KKKT Dayosisi ya Kusini

14.    Askofu Dk. Hance Mwakabana, KKKT Dayosisi ya Kusini Kati

15.    Askofu Job T. Mbwilo, KKKT Dayosisi ya Kusini Magharibi

16.    Askofu Zebedayo Daudi, KKKT Dayosisi ya Mbulu

17.    Askofu Paulo Akyoo, KKKT Dayosisi ya Meru

18.    Askofu Jacob Mameo Ole Paulo, KKKT Dayosisi ya Morogoro

19.    Msaidizi wa Askofu Mchg. Eliraha Mmwiri, KKKT Dayosisi ya Pare

20.    Askofu Renard K. Mtenji, KKKT Dayosisi ya Ulanga Kilombero

 

Dodoma
7 Januari 2010

 

==================================================
Elizabeth Lobulu
Communication Coordinator,
Evangelical Lutheran Church in Tanzania
Box 3033, ARUSHA, Tanzania.
Phone: +255-27-250-8856/7
FAX: +255-27-254-8858
E-mail: Elizabeth Lobulu <ELobulu@elct.or.tz>

Close this window

For more information contact:

Elizabeth Lobulu
Communication Desk Officer, ELCT
E-mail: ELobulu@elct.or.tz