ELCT Press Release
Date: Desemba 11, 2010
Press release No. 002/12/2010

Killewa ampongeza Malasusa kwa kuthibitishwa kuendelea kuongoza Dayosisi yake (English)

Katibu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Bw. Brighton Killewa, amempongeza Askofu Dkt. Alex Malasusa kwa kuthibitishwa kuendelea kuongoza Dayosisi ya Mashariki na Pwani hadi atakapostaafu na kusema kwamba wana-KKKT wana imani na uongozi wake.

Katika taarifa aliyoitoa 11 Desemba 2010 kwa vyombo vya habari, alisema: "Imani iliyooneshwa na Dayosisi yake kwa kumthibitisha aendelee kuwa Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani mpaka atakapostaafu ni kubwa na inawakilisha maoni ya wana-KKKT wote."

Askofu Malasusa ambaye pia ni Mkuu wa KKKT alithibitishwa na Mkutano Mkuu wa 30 wa Dayosisi yake baada ya kuiongoza kwa miaka sita.

Katiba ya Dayosisi hiyo inataka Askofu akishachaguliwa atumikie Dayosisi kwa miaka sita na ndipo Mkutano Mkuu unapoitwa ufanye kura ya imani ili aendelee kuongoza Dayosisi hadi atakapofika umri wa kustaafu au la kumbadilisha kwa kura ya kutokuwa na imani naye.

Kura ya imani ilipopigwa kwa ajili ya Askofu Malasusa, alizoa asilimia 96.6 ya kura zilizopigwa za wajumbe 265.

Neno Kuu la Mkutano huo uliofanyika Bagamoyo tarehe 5 - 8 Desemba 2010 lilikuwa: "Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu." (Yohana 12: 32).

Tarehe 29 Novemba 2010 Kamati ya Utendaji ya KKKT kwa niaba ya Halmashauri Kuu ilitoa tamko linalopinga tuhuma zenye lengo la kumchafua Askofu Dkt. Malasusa zilizotolewa kwenye magazeti ya Rai na Mtanzania yanayomilikiwa na Kampuni ya New Habari Corporation.

Lifuatalo ni tamko hilo kwa vyombo vya habari:

KANISA LA KIINJILI LA KILUTHERI TANZANIA

TAMKO LA KAMATI YA UTENDAJI YA HALMASHAURI KUU YA KANISA
KUHUSU MAKALA ZILIZOTOLEWA KWENYE MAGAZETI

Kamati ya Utendaji ya Halmashauri Kuu ya Kanisa iliyofanya mkutano tarehe 29 Novemba 2010 Arusha, pamoja na mambo mengine ilijadili tuhuma zenye lengo la kumchafua Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani na Mkuu, KKKT Mhe. Askofu Dk. Alex Malasusa zilizotolewa kwenye magazeti ya Rai na Mtanzania yanayomilikiwa na Kampuni ya New Habari Corporation.

Kufuatia tuhuma zilizotolewa kwenye magazeti hayo na wanaojiita wakereketwa /washarika wa KKKT-DMP, Kamati ya Utendaji ya Halmashauri Kuu ya Kanisa inatoa tamko kama ifuatavyo hapa chini:-

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), na hata KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, hawajawahi hata siku moja kupokea tuhuma dhidi ya Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Askofu Dk. Alex Malasusa ambaye pia ni Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, kwa mujibu wa kanuni na taratibu zilizowekwa na Kanisa.

Watoa tuhuma hizo kwenye magazeti ambao hawafahamiki hawana hoja, bali ni wazushi na waongo, wenye nia yao binafsi, ndio maana wanakimbilia kwenye magazeti. Kwa mfano, kutoa tuhuma yenye mwelekeo wa kuharibu uhusiano kati ya Serikali na Kanisa haina msingi wo wote. Hatuamini kuwa Serikali yetu imekosa watu wa kuisemea kiasi cha kusemewa na watu hawa wasiojulikana.

Ni vema Kanisa na jamii kwa ujumla wake iwapuuze watu wa jinsi hiyo, ambao wana chuki binafsi au wanatumiwa na watu wenye chuki au nia mbaya dhidi ya Kanisa, ambao furaha yao ni kuona Kanisa linaingia kwenye mgogoro, na pia kuliondoa Kanisa katika malengo yake ya kuihubiri Injili ya wokovu kwa watu na kuwasaidia katika mahitaji yao ya kimwili na kiakili ambayo yamekuwa yakitekelezwa na kufanyiwa kazi na uongozi thabiti wa Askofu Dk. Alex Malasusa.

Mwisho Kwa niaba ya Ofisi Kuu ya KKKT, napenda kumpongeza Baba Askofu Dk. Alex Malasusa kwa kuthibitishwa na Dayosisi ya Mashariki na Pwani kuwa Askofu wake mpaka atakapostaafu. Imani iliyoonyeshwa na Dayosisi yake ni kubwa na inawakilisha maoni ya wana KKKT wote.

Bw. Brighton B.L. Killewa
Katibu Mkuu, KKKT

Arusha, 11 Desemba 2010



Issued by the:
Secretary General's Office, ELCT.

==================================================
Elizabeth Lobulu
Communication Coordinator,
Evangelical Lutheran Church in Tanzania
Box 3033, ARUSHA, Tanzania.
Phone: +255-27-250-8856/7
FAX: +255-27-254-8858
E-mail: Elizabeth Lobulu <ELobulu@elct.or.tz>

Close this window

For more information contact:

Elizabeth Lobulu
Communication Desk Officer, ELCT
E-mail: ELobulu@elct.or.tz